Kwa mujibu wa Idara ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Ibrahim Zakzaky aliyasema hayo katika hafla ya Maulidi ya Mtume wa Rehema (saww), iliyoandaliwa na Jumuiya ya Rasilimali ya Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, “Resource Forum”. Hafla hiyo ilifanyika Jumapili, tarehe 22 Shahrivar 1405, sawa na tarehe 1 Rabiul Thani 1448.
Kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, katika hotuba yake alisisitiza umuhimu wa umoja wa Waislamu na kurejea katika mafundisho ya Mtume wa Rehema (saww), akisema: “Mtume alileta kwa watu dini iliyokamilika na yenye kujumuisha kila jambo, na akaijenga jamii kwa misingi yake; wajibu wetu ni kuifuata.”
Akiashiria juhudi za maadui za kudhoofisha nafasi ya Mtume wa Rehema (saww), alisema: “Maadui wanajaribu kuichafua na kuipotosha sura ya Mtume (saww), kwa sababu wamegundua kwamba Waislamu wamemkubali Mtume wa Uislamu (saww) kuwa ni alama ya umoja na mshikamano wao.”
Sheikh Zakzaky pia alionya kuhusu migawanyiko na migogoro inayozushwa miongoni mwa Waislamu, huku akasisitiza: “Migawanyiko inayozushwa miongoni mwa Waislamu kwa jina la dini au ukabila haina faida yoyote kwa Umma wa Kiislamu; bali inawanufaisha tu maadui ambao huzusha migawanyiko hiyo kwa ajili ya kutimiza maslahi yao.”
Akaongeza kusema: “Maadui, kwa kuzusha migogoro na ukosefu wa usalama, wanajaribu kugeuza fikra za watu kutoka katika masuala ya msingi; wakati ambapo katika mazingira hayo hayo, utajiri wao unaporwa na watu wanazidi kutumbukia katika umaskini na mifarakano.”
Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amesisitiza: “Kuzitambua mbinu hizi za maadui, kuimarisha umoja miongoni mwa Waislamu na kurejea katika mafundisho halisi ya Mtume wa Rehema (saww), ni miongoni mwa njia muhimu zaidi za kutatua matatizo ambayo Umma wa Kiislamu unakabiliana nayo.”
Hafla hii, ambayo “Resource Forum” ya Harakati ya Kiislamu ya Nigeria huandaa kila mwaka, ilihudhuriwa na makundi mbalimbali ya Waislamu, wakiwemo Maimamu wa misikiti, wanazuoni, wafanyakazi na makundi mengine ya jamii.
Maoni yako